NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA KWANZA
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU
SIKU YA KWANZA, IJUMAA
ROHO MTAKATIFU ANATUFARIJIYesu alipokuwa akiagana na mitume wake, kabla ya kupaa mbinguni, aliwaambia wasiondoke Yerusalemu mpaka hapo watakapokuwa wamempokea Roho Mtakatifu. Aliwaambia: “Wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni, mtajazwa nguvu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika nchi yote ya Yuda na Samaria, hata kwenye mipaka yote ya dunia.” (Mdo.1:8)
Waliendelea kusali pamoja toka hapo Yesu alipopaa mbinguni mpaka siku ya Pentekoste. Waliomba Roho Mtakatifu awashukie, awajaze na mapaji yake. Na baada ya siku tisa Roho Mtakatifu aliwashukia hao kundi dogo nao wakawa chanzo cha Kanisa lililopata kuenea duniani kote.
Siku hizo tisa za kusali zinaitwa NOVENA; na kila mwaka wakati huu, wakristu wakifuata mfano wa mitume, wanasali muda wa siku tisa kabla ya Sikukuu ya Pentekoste. Wanamuomba Roho Mtakatifu awashukie, awajaze nguvu na wingi wa mapaji yake.
Wakati huu wa NOVENA , Tunayo mengi ya kuliombea Kanisa na kujiombea sisi wenyewe. Kwa hiyo tumuombe Roho Mtakatifu atusaidie kusali vema na kuomba yale yote tunayohitaji kwa maslahi yetu ya roho na mwili.
Na kama mtume Paulo alivyowaambia wale waKristu wa kwanza, Roho Mtakatifu huja kutufatiji katika udhaifu wetu. Basi tumuombe atufariji kwa sala hizi za NOVENA, Atuwezeshe kusali na kuomba inavyotupasa kusali.
1. Ee Baba wa milele, tunakuomba umtume Roho Mtakatifu atushukie sisi taifa lako awashe ndani yetu moto wa upendo wako.
W. Twakuomba utusikie.
2. Ee Baba mwema, tunakuomba utujalie faraja ya Roho Mtakatifu sisi wana tulio katika dhiki na taabu nyingi mno hapa duniani.
W. Twakuomba utusikie.
3. Ulijalie Kanisa lako mapaji ya Roho wako Mtakatifu, liweze kutekeleza vema utume wake wa kuhudumia watu wote hapa duniani.
W. Twakuomba utusikie.
4. Utujalie sisi kudumu katika NOVENA hii mpaka mwisho kama Maria na mitume walivyodumu pamoja wakisali kabla ya Pentekoste ile ya kwanza.
W. Twakuomba utusikie.
5. Utujalie neema zote zinazohitajika ili tuweze kumshuhudia Kristu popote kwa mwenendo na matendo yetu ya kila siku, tukiongozwa na Roho Mtakatifu.
W. Twakuomba utusikie
6. Uzijalie familia zote za wakristu neema na nguvu za Roho Mtakatifu tupate kuendelea pasipo kuchoka katika sala na katika matendo mema siku zote.
W. Twakuomba utusikie
7. Ewe Roho Mtakatifu, uwajalie vijana wetu moyo wa ujasiri, wapate kulijenga kanisa lako na kueneza utawala wako katika jumuia zetu za Kikristu.
W. Twakuomba utusikie.
TUOMBE;
Ee Mungu, uliye muumba wa vitu vyote , tunakuomba utusikilize kwa wema sala zetu sisi taifa lako, utuongoze sote tufuate siku zote utaratibu wa mapenzi yako; naye Roho Mtakatifu atutegemeze mpaka mwisho wa novena hii. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu .
W. Amina.
LITANIA YA ROHO MTAKATIFU
Bwana Utuhurumie………Utuhurumie
Kristu utuhurumie……..….Utuhurumie
Bwana utuhurumie….. Utuhurumie
Baba mweza wa vyote….. Utuhurumie
Yesu Mwana wa Pekee wa Baba na Mwokozi wa Dunia……..Utuokoe
Roho wa Baba na Mwana aunganishaye maisha ndani ya Baba na Mwana………….Ututakatifuze
Roho Mtakatifu……….Utusikie
Roho Mtakatifu atokaye kwa Baba na Mwana…………..Njoo ndani ya mioyo yetu
Ahadi ya Mungu Baba……………… Njoo ndani ya mioyo yetu
Mionzi ya Mwanga kutoka Mbinguni……………… Njoo ndani ya mioyo yetu
Mwandishi wa vyote vilivyo vizuri……………… Njoo ndani ya mioyo yetu
Chanzo cha Maji ya Uzima……………… Njoo ndani ya mioyo yetu
Moto utumikao daima……………… Njoo ndani ya mioyo yetu
Muungano Mtakatifu……………… Njoo ndani ya mioyo yetu
Roho wa ukweli na upendo……………………Utuhurumie
Roho wa hekima na elimu……………………Utuhurumie
Roho wa shauri na nguvu……………………Utuhurumie
Roho wa akili na neema ya kumtumikia Mungu……………………Utuhurumie
Roho wa neema na sala……………………Utuhurumie
Roho wa amani na subira……………………Utuhurumie
Roho wa usafi na uaminifu……………………Utuhurumie
Kitulizo cha Roho……………………Utuhurumie
Roho aletaye Utakatifu……………………Utuhurumie
Roho uongozaye Kanisa……………………Utuhurumie
Zawadi kutoka kwa Mungu juu Mbinguni……………………Utuhurumie
Roho ajazaye ulimwengu……………………Utuhurumie
Roho Mtakatifu…………………..tupe neema ya kuchukia dhambi
Roho Mtakatifu…………………..njoo ufanye upya sura ya ulimwengu
Roho Mtakatifu…………………..jaza roho zetu kwa mwanga wako
Roho Mtakatifu…………………..ifuraishe mioyo yetu kwa sheria yako
Roho Mtakatifu…………………..washa moto wa mapendo ndani yetu
Roho Mtakatifu…………………..jaza mioyo yetu na hazina ya neema yako
Roho Mtakatifu…………………..tufundishe kusali vyema
Roho Mtakatifu…………………..tuangaze kwa nguvu zako za Ki-Mungu zitupatiazo moyo wa kutenda daima yaliyo mema
Roho Mtakatifu…………………..tuongoze Kwenye njia ya wokovu
Roho Mtakatifu…………………..tuweze kufahamu yale ya muhimu tu
Roho Mtakatifu…………………..tupe hamu ya kuitafuta fadhila yako
Roho Mtakatifu…………………..tusaidie tuweze Kupata fadhila zote
Roho Mtakatifu…………………..tupe uvumilivu tuweze kutenda yaliyo mema tu.
Roho Mtakatifu…………………..tunaomba uwe zawadi ya uzima wetu
Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia…………….Tushushie Roho wako Mtakatifu
Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia…………….jaza mioyo yetu kwa mapaji yako ya Roho Mtakatifu
Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia…………….tupe roho ya hekima na neema ya kumsifu Mungu.
Njoo Roho Mtakatifu uzijaze roho za waumini wako uwashe moto wa mapendo yako ndani ya mioyo yetu
TUOMBE
Ee Mungu Baba mwenye huruma tujalie Roho wako alete Mwanga kwetu ili apate kututakasa na kuingiza ndani ya mioyo yetu Baraka za kuweza kutenda yale yaliyo mema.
Tunaomba hayo kupitia kwa Mwanao Mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo, anbaye anaishi na kutawala pamoja nawe katika Umoja wa Roho Mtakatifu. AMINA
Atukuzwe Baba…..x3
Comments
Post a Comment